Maisha yako. Chagua lako.
Habari WanaSpringsters
Hakuna jambo gumu kuliko kuchagua kati ya njia ambayo wazazi wetu wanataka tufuate na njia tunayotaka wenyewe.
Nawapenda wazazi wangu sana, naamaanisha damu yao inapita ndani ya mishipa yangu – uhusiano wa karibu kabisa. Hata hivyo, ni muhimu kukumbuka kwamba sisi ni watu tofauti, wenye akili na mioyo tofauti.
Sikuwahi kuwaeleza wazazi wangu kuhusu ndoto yangu ya kuwa mwandishi kwa sababu walitaka nifanye vizuri katika hesabu na kufanya kazi kama kashia katika duka la karibu. Walisema makashia hulipwa vizuri na hilo lingeleta sifa nzuri kwa familia yetu.
Kwa kuwa niliwapenda sana, nilipuuza ndoto zangu na kufuata kile walitaka. Niliwaruhusu kufanya maamuzi yote na nikabaki kimya.
Jioni badala ya kufanya mazoezi ya uandishi bunifu, nilifanya hesabu. Shuleni nikatilia mkazo somo la hesabu na biashara badala ya fasihi na unandishi bunifu. Hatimaye nilipata kazi kama kashia, nilifurahi kwa sababu wazazi wangu wangejivunia mimi, lakini siku zilipoendelea kupita nikaanza kupoteza furaha.
Kuzungumzia kuhusu kile unataka si rahisi lakini inawezekana. Nikiangalia nyuma, najuta kuwa sikusema nilichotaka na na kuzungumza na wazazi wangu kuhusu uamuzi huo. Ndio, wazazi wako hapa kutusaidia kufanya uamuzi bora lakini una jukumu la muhimu wanapofanya maamuzi yanayokuhusu.
Zungumza na kufuata moyo wako kwa sababu maoni yako ni ya muhimu. Usingoje ifike wakati ambapo utaanza kujutia kwa sababu ya mambo ambayo hukufanya, ilhali una nafasi ya kuzungumza sasa.
Nimeanza kufuata ndoto zangu kwa kuandika mashairi mafupi. Nitakapokuwa tayari nitawapa wazazi wangu ili wasome na kuzungumza nao kuhusu shauku yangu ya kweli ya uandishi.
Kumbuka: Usijiwekee mzigo mzito kwa kufuata njia "sahihi". Maisha ni safari na sio mbio. Kwa hivyo hata ukifuata njia fulani kisha ugundue huipendi, una nafasi ya kugeuka na kufuata njia nyingine. Hujachelewa kufuata ndoto zako.
Share your feedback