Niliolewa nikiwa mchanga

…Lakini bado natimiza ndoto zangu.

Vipi wasichana,

Jina langu ni Ruth na niliolewa nikiwa mchanga! Baada ya kumaliza masomo ya sekondari, wazazi wangu walinitafutia bwana na nikaolewa. Mwanzoni ilikuwa raha, lakini baadaye maisha yangu yakageuka kuwa desturi: kuamka, kumtayarisha mume wangu kwenda kazini, kufanya kazi za nyumba, kula na kisha kwenda kulala.

Niliwaza mara nyingi, “Hivi ndivyo maisha yangu yote yatakuwa au bado ninaweza kutimiza ndoto zangu za kuwa mwalimu?”

Jioni moja baada ya chakula cha jioni, nilimpeleka mume wangu mahali tulipopapenda na nikamwambia kwamba nilitaka kuwa mwalimu. Alikataa na kusema kwamba ingekuwa kazi nyingi sana kwangu. Mazungumzo yakawa magumu na hatukuweza kuafikia makubaliano. Niliamua sitapaza sauti yangu au kuendelea na mabishano yale.

Baadaye wiki ile, niliamua kumuuliza mama yangu ushauri. Daima yeye hunisaidia ninapohitaji kufanya maamuzi magumu.

Mama yangu aliniambia kwamba ndoa ni ngumu na wakati mwingine watu hawakubaliani, hasa inapokuja ni wakati wa wanawake kufuatilia ndoto zao. Aliniambia kwamba kwa sababu lilikuwa ni jambo muhimu kwangu, nijaribu kuanzisha mazungumzo yale tena na nimsaidie mume wangu kuona umuhimu wa mimi kutimiza ndoto zangu. Kwa mfano, ninaweza kusaidia familia yetu kifedha, nitaweza kuelewa shinikizo zake za kazi vyema na pia ningeweza kumpa ushauri bora zaidi. Pia kwa vile tutakuwa sote tuna mapato tutaweza kuweka pesa fulani kando ili kuweka akiba ya siku za baadaye za familia yetu.

Mama yangu alinipa vidokezo hivi vitatu vya kuwa na mazungumzo magumu;

  1. Hakikisha uko pahali patulivu.
  2. Tafuta mada ambayo inavutia kila mtu ili kutengeneza mpatano na mazungumzo rahisi.
  3. Eleza hoja yako kwa uwazi, hata ikiwa ngumu, kumbuka kwamba usipaze sauti yako.

Nilizingatia ushauri wa mamangu. Mume wangu alionekana kukubali wazo langu kuwa mwalimu na akasema angelifikiria. Baada ya muda, alibadili nia na akanisaidia kabisa!

Sasa ninajua kwamba kama una ndoto unaweza kuitimiza hata kama uliolewa ukiwa mchanga, unapaswa tu kupata mtu anayefaa kukupa ushauri na kukusaidia.

Share your feedback