Kuweka pesa akiba kunaweza kuwa jambo la kufurahisha, jaribu vidokezo hivi vizuri
Kutenga pesa kunaweza kuwa rahisi kusema lakini si rahisi kutenda. Hapa kuna vidokezo vya kukusaidia unapoendelea:
Wakati wote jibebee chakula cha mchana
Unaweza kununua chakula cha mchana au vitafunwa shuleni lakini ukipika nyumbani itakuwa rahisi zaidi na bora kwa afya yako. Ikiwa unajaribu kuokoa pesa zako, kula nyumbani kabla kwenda kutangamana na marafiki zako. Agiza kinywaji au kitafunwa kidogo wakati unapokwenda kula nje – kwa njia hiyo utatumia pesa kidogo.
Ufanye mtumba uwe rafiki yako
Usiogope kuvaa nguo za mtumba, kusema kweli kuvaa nguo hizo ndio mtindo sasa hivi hususan kama unajua kuchagua vizuri! Tafuta zile nguo ambazo dada yako mkubwa, mama yako, au shangazi zako hawazivai tena. Nguo za zamani zinaweza kuwa nzuri sana haswa ukizichanganya na za kisasa. Tafuta sindano au cherahani pia, utakuta kwamba vitu vingi vinahitaji kushonwa kidogo tu na virudi kuwa vizuri kama zamani.
Usiende madukani, sokoni na majumba ya mauzo
Unapojaribu kuweka akiba, hata kwenda kuangalia vitu dukani ni vibaya, hususan ikiwa unapenda kununua vitu wakati una usongo wa mawazo, umekasirika au una huzuni. Ni kweli kwamba watu wengi hutumia pesa zaidi kwa kununua vitu wasivyovihitaji wakati wamejawa na hisia.
Kusanya sarafu ulizokuwa umeziacha
Sisi sote huwa tuna sarafu katika pochi zetu. Jaribu kuziweka sarafu hizo kwenye chombo fulani. Mara watu wanapojua kwamba unakusanya sarafu utashangaa ni watu wangapi watapenda kukupa sarafu zao. Unapokuwa na sarafu za kutosha, zibadilishe kwa noti katika duka la kubadilisha pesa au ziweke benki ili usiweze kuzitumia.
Jiepushe na madeni
Kukopa pesa kwa ajili ya kujifurahisha na kununua vitu vizuri vizuri ambavyo haviwekezi katika maisha yako ya baadaye kama shule au vitabu ndivyo mazoea mabaya ya kutumia pesa vibaya huanzia. Watu wenye madeni yasiyokuwa ya lazima ni nadra kufaulu katika maisha – yaepuke na uwe na subira. Ikiwa unaitaka, iweke akiba, hatimaye utakuwa na pesa zaidi mbeleni.
Share your feedback