Kwa nini ni muhimu
Ukiwa na pesa, inaweza kuwa rahisi zaidi kuzitumia! Haswa ikiwa kuna kitu ambacho umekuwa ukikitaka kwa muda mrefu – kama vile kitambaa cha kushona sketi mpya au kitabu cha riwaya cha mwandishi wako unayempenda. Kujinunulia kitu wakati mwingine si vibaya, lakini kuweka akiba ya baadaye ni muhimu sana.
Kuweka akiba hata kidogo unapopata pesa ni njia ya kufanya kitu bora kwa maisha yako ya baadaye. Lakini huwa si rahisi wakati wote, kwa hivyo hii hapa ni jinsi ya kuanza:
Fanya hesabu ya ni pesa ngapi unazohitaji sasa hivi – ikiwa lazima ununue vitabu vya shuleni au mahitaji mengine, kama dawa, ni sawa kutumia hela. Kutoka hapo, unaweza kutenga pesa kidogo ya kujishughulikia – labda sabuni bora mpya. Nyingine zinazosalia ndizo utakazoweka akiba. Kiasi gani kinatosha? Jaribu kuweka angalau nusu ya kile ulicho nacho.
Zungumza na wazazi wako au mtu mzima anayeaminika kama shangazi kuhusu kufungua akaunti kwenye benki au kikundi cha karibu cha akiba. Baadhi ya vikundi vya akiba vinaweza kukuruhusu kufungua akaunti yako binafsi lakini vingine vinaweza kuruhusu mtu mzima tu akufungulie akaunti. Jambo zuri kuhusu kuweka pesa zako mbali hivi ni kuwa itakuhitaji kutumia nguvu kuzifikia – na kuzitumia!
Ikiwa huwezi kufika benkini, tumia mkebe, kopo, au kikasha kilichotumika chenye kufuli kuweka pesa zako ndani ili ziwe mbali nawe. Waombe wazazi wako wakuekee mkebe huo au uuhifadhi katika eneo salama ambapo huwezi kuufikia kwa urahisi – hii itakurahisishia kutotumia pesa!
Kuweka akiba ni muhimu kwa siku zako za usoni – na ni tabia nzuri ya kuanza sasa. Mambo mengi makubwa unayoweza kuhitaji maishani – kama kusoma, kufungua biashara, hata kuolewa au kununua nyumba siku moja – yanaweza kugharimu hela nyingi. Kwa kujifunza jinsi ya kutenga pesa sasa, itakuwa rahisi kumudu gharama kubwa ya maisha itakapofika baadaye!
Share your feedback