Fuata hatua hizi 3
Hujambo dada!
Shinikizo kutoka kwa marafiki linaweza kukithiri! Je, umewahi kuwa katika hali ambapo hukutaka kufanya jambo lakini uliishia kulifanya, hasa kwa kuwa kila mtu mwingine alikuwa akilifanya? Unajua nini? Sote tumepitia hili! Kujifunza kusema HAPANA sio kibarua rahisi lakini ni stadi ambayo sote tunaweza kujenga na kufanya.
Hatua 1 – Epuka kujitia katika hali ngumu
Tuseme hauko tayari kushiriki ngono lakini mvulana anakualika katika chumba chake “mkatulie” usiku wa manane. Unajua kwamba ana hamu ya kushiriki ngono lakini hauko tayari kushiriki. Utafanyaje?
A: Utaenda katika chumba chake usiku wa manane
B: Utasema HAPANA na umwombe mkutane mahali hadharani.
Jibu sahihi ni B! Iwapo utaweza kuepuka hali ngumu, basi ziepuke. Majuto sio hisia nzuri, kwa hivyo iwapo tunaweza kuyaepuka kwa kufanya maamuzi mazuri basi hiyo ni hatua nzuri. Usitumie muda wako na watu ambao hukufanya uwe na wasiwasi au hukushinikiza kufanya mambo ambayo hauko tayari kushiriki.
Hatua 2 – Wazia matokeo ya matendo yako
Wakati uko karibu kusema NDIYO au HAPANA kwa uamuzi wowote, usifuate hisia zako pekee. Chukua muda kutafakari vizuri kuhusu kitakachotokea baada ya uamuzi wako. Iwapo umeridhika na matokeo, basi sawa. Iwapo haujaridhika na matokeo yanayowezekana, basi kuwa mjasiri na useme HAPANA na ugeuze nia.
Kwa mfano, kuna hatari za kihisia za kushiriki ngono mapema kama vile majuto, wasiwasi na kuchanganyikiwa. Pia unaweza kushika mimba iwapo hautatumia kinga. Kwa hivyo iwapo hauko tayari kukumbana na hali hizi, kusema HAPANA ndio jambo la busara kufanya.
Hatua 3 – Ongea na Ujitetee
Sauti yako ni muhimu. Mawazo yako ni muhimu. Usimruhusu yeyote akufanye ubadilishe mawazo haya. Una uwezo wa kuchagua na kuamua kile unachotaka kufanya na maisha yako. Kwa hivyo kuwa mwaminifu kwa nafsi yako.
Tuchukulie uliamua kuchukua jibu A na ukaenda katika chumba cha mvulana usiku wa manane. Iwapo atakuomba kushiriki ngono na hutaki, una haki ya kusema HAPANA.
Ni mwili wako kwa hivyo una haki ya kuamua. Haimanishi kwamba kwa sababu umeenda katika chumba chake basi ana haki ya kushiriki ngono nawe.
Kutetea kile unachoamini ni muhimu. Usinyamaze iwapo kuna kitu ambacho hukubaliani nacho.
Huenda kusema HAPANA ni vigumu, lakini ni muhimu kujitetea na kufanya yale tu unayohisi ni sawa kwako.
Share your feedback