Je, umewahi kusikia kuhusu Maambukizi ya Zinaa?
Unajua nini? Mimba sio matokeo pekee ya ngono bila kinga.
Iwapo utashiriki ngono bila kondomu, upo katika hatari ya kupata maambukizi ya zinaa (almaarufu STI). Maambukizi ya zinaa ni maambukizi yanayotokana na mgusano wa kingono.
Baadhi ya dalili za maambukizi ya zinaa ni:
Baadhi ya maambukizi ya zinaa yana dalili zinazoonekana huku mengine yakiwa na dalili zisizoonekana moja kwa moja. Mifano ya maambukizi ya zinaa ni kama klamedia, kisonono na hata UKIMWI. Iwapo hujui kwamba umeambukizwa, unaweza kusambaza maambukizi kwa mpenzi wako.
Maambukizi ya zinaa yasiyotibiwa yanaweza kusababisha madhara zaidi na magonjwa. Hii ndio maana ni muhimu kuujua mwili wako, na kujua nini cha kawaida na kizuri kwako. Wakati kitu kinaonekana tofauti, tembelea daktari.
Namna ya kuzuia maambukizi ya zinaa
Kutumia kondomu ndio njia bora zaidi ya kuzuia maambukizi ya zinaa kwa kuwa sio njia zote za kupanga uzazi zinakukinga. Kwa mfano, hata kama unatumia tembe kuzuia mimba, haitakuzuia kupata maambukizi ya zinaa. Kwa hivyo unapowazia upangaji uzazi kumbuka kuuliza kuhusu viwango vya kinga unavyopata. Zungumza na mtu unayemwamini kama vile mamako, shangazi au mhudumu wa afya ili kujua mengi zaidi.
Upo katika uhusiano wa kimapenzi? Endelea kusoma!
Mojawapo wa mambo muhimu zaidi kuhusu afya ya ngono ni jinsi wewe na mpenzi wako mnawasiliana. Unapokuwa tayari kushiriki ngono, hakikisha mna uwazi kuhusu historia yenu ya ngono. Iwapo mpenzi wako amewahi kuwa na maambukizi ya zinaa hapo awali unahitajika kujua na yeye pia anahitaji kujua historia yako.
Kabla hujaingia katika uhusiano unaojumuisha ngono, ni wazo zuri kwenu nyote kutembelea kliniki na kupimwa. Hivi, mnaweza kujua iwapo mmoja wenu ana maambukizi ya zinaa. Kinga ni bora kuliko tiba.
Iwapo unafikiri kuwa kuna uwezekano mkubwa una maambukizi ya zinaa, usihofu. Tembelea kliniki au hospitali upate kupimwa. Tafuta daktari anayeaminika na unayehisi salama kwake. Mweleze ukweli ili upate dawa na tiba inayostahili.
Unachukua hatua inayofaa kwa kutafuta msaada wa mtaalamu na hivyo hufai kuona aibu. Maambukizi ya zinaa yanaweza kutibiwa kwa urahisi kwa kutumia dawa zinazofaa.
Share your feedback