Pole… Kijana!

Wakati kila mtu anapogundua mwili wako unabadilika

Kwa heri kaka! Ndivyo nilimwambia alipojaribu kunisemesha baada ya miaka kadhaa. Je, ungetaka kujua sababu? Endelea kusoma.

Niliskia vitu vingi kuhusu ubalehe nilipokuwa ninakua. Mwili unabadilika, unaanza hedhi, homoni zinaongezeka na vitu kama hizo. Lakini hakuna mtu alinionya kuwa watu wataanza kuniangalia angalia. Na ndio sababu nataka kushiriki stori yangu na wewe.

Kulikuwa na huyu kaka mtaani kwetu – Zain. Nilitamani sana kuwa demu wake kwa miaka mingi, lakini hakushughulika na mimi. Nilijaribu kuongea na yeye mara kadhaa, lakini alikatisha mazungumzo na hata kujifanya hakunisikia. Hii ilikuwa ishara kuwa hakunitaka. Hivyo mimi nikasare na kuendelea na maisha.

Mwaka jana, niliongezeka ukubwa. Nilianza kuona matiti yangu yakiwa makubwa, hipsi zilianza kuonekana na makalio pia! Lakini sikuwa mimi pekee niliyekuwa naona mabadiliko haya. Baada ya miaka mingi ya kunipuuza, Zain alianza kunisalimia tena. Kwanza ilikuwa “mambo” kisha akaanza kusema jinsi nilivyokuwa “mdada mkubwa” sasa nilikuwa naonekana mrembo. Akaanza kujaribu kuniambia nisiende shule, niwe naye, lakini sikutaka. Lakini hakuwa peke yake. Ni kama kila mtu alitaka kuniambia vile mwili wangu ulikuwa unabadilika.

Ni kweli, naweza kuwa dada mkubwa sasa, lakini pia mi ni mjanja na nina ndoto kubwa. Sikuwa tayari kuruhusu anichanganye nisifikie malengo yangu. Hasa nilipofikiria nia yake haikuwa ya kweli. Nilimwambia, Kwa heri – Kaka!

Sikua na mtu wa kuongea naye nilipokuwa napitia haya, hivyo nikasema lazima nishiriki stori yangu na dada yangu mdogo na marafiki zake walipoanza kupitia haya. Ukiongea kuhusu mabadiliko unayopitia na kushiriki stori yako huwa inakusaidia sana na hata husaidia watu wanaokusikiliza. Na sababu sasa dadangu na marafiki zake wanajua zaidi, wanaweza kufanya maamuzi bora. Hivo ninapogundua kitu kunihusu na katika mwili wangu, sina shida kueleza wengine ikiwa najua kitawasaidia pia!

Share your feedback