Maisha hayafuati mipango yetu kila wakati, lakini palipo na nia, pana njia
Sisi Springsters tunajua kuwa ni muhimu kuweka mipango kwa siku zetu za usoni, lakini ni nini ambacho hutokea wakati ambapo kila tulichopanga hugeuzwa juu chini ghafla?
Sasa hivi, maisha yanaweza kuwa ya kutisha kidogo na yasiyoweza kutabirika. Wakati mwingine maishani, haijalishi tunavyopanga na kujitayarisha, mambo hayatatokea jinsi tulivyotarajia.
Ilahali ni kawaida kuwa na wasiwasi, huzuni, au hata kukasirika kuhusu changamoto zisizotarajiwa zinazojitokeza maishani, changamoto hizo hizo ni fursa ya kuimarika na kuonyesha ulimwengu jinsi sisi wasichana tulivyo thabiti.
Hii hapa ni hadithi kuhusu msichana kwa jina Muji. Muji alipokuwa katika mwaka wake wa mwisho wa shule ya upili, ilionekana kama ndoto yake kuu ilikuwa inakaribia kutimia: akakubaliwa chuoni!
Kama msichana mdogo aliyelelewa katika kijiji chake kidogo, Muji alikuwa na ndoto ya siku moja kwenda mjini na kujiunga na chuo. Alikuwa na shauku sana, lakini baada ya kuzungumza na wazazi wake, aligundua kuwa hawakuwa na pesa zozote za kumlipia ada ya masomo.
Muji aliumia. Alikaa kwa muda akihisi kuvunjika moyo, kukasirika, na kusikitika. Baada ya muda, aliamua kutumia nguvu zake kutayarisha mpango: iwapo wazazi wake hawangemlipia karo ya chuo, angetafuta jinsi ya kujilipia.
Muji alituma jibu kwa chuo na kuwaambia kuwa alihitaji kuahirisha kujiunga kwake na, mara alipokamilisha masomo yake ya shule ya upili, alianza kutafuta kazi.
Mwishowe alipata nafasi katika kituo ndogo cha redio katika mji uliokuwa karibu na akafanya kazi kwa mwaka kama mwanahabari mdogo huku akiwa anaziweka pesa zake zote kama akiba.
Baada ya mwaka mmoja wa kufanya kazi kwa bidii na kuweka akiba nyingi, Muji alikitumia chuo ujumbe kuhusu kujiunga kwake, na akaamua kutuma ombi la msaada wa masomo ili kumsaidia kulipa ada ya masomo. Unajua nini?! Bidii yake ilimlipa! Alikuwa anaelekea kujiunga na chuo NA alikuwa amepata ufadhili kamili wa masomo!
Ilikuwa vigumu kwa Muji kuamini kuwa hakika hii ilikuwa ikitokea, lakini alijua kuwa bado alikuwa na kazi nyingi mbele yake: ufadhili wake wa masomo ulikuwa unalipa tu ada ya masomo, na maisha jijini yangekuwa ghali. Je, angeishi vipi?
Muji alipata barua ya marejeo kutoka kwa stesheni ya redio ya kuonyesha kuwa alikuwa akifanya kazi pale na akaitumia kupata kazi ya muda katika stesheni ya radio ya chuo chake. Aliajiriwa! Mshahara huo, pamoja na pesa alizopata kutokana na kufanya kazi zingine za pembeni, zilitosha kugharamia gharama zake za kuishi.
Muji alikuwa mtu wa kwanza katika familia yake kujiunga na chuo, na alifanya hivyo kwa juhudi zake mwenyewe! Baada ya kuhitimu, Muji aliitumia tajriba yake ya kazi kumsaidia kupata kazi kama mwandishi wa kitaalamu katika mji mkuu. Hakika bidii yake ilikuwa imemlipa!
Ingawa alikuwa amekasirika na kusikitika, ni changamoto na vikwazo hivyo hivyo ambavyo hakika vilimsaidia Muji kuzitimiza ndoto zake.
Iwapo asingechelewesha kujiunga na chuo na kufanya kazi kwa mwaka, huenda asingepata ufadhili wa masomo. Na iwapo hakuwa na tajriba ya kazi katika kijiji chake, huenda asingepata kazi katika kampasi ya chuo chake. Na iwapo hakuwa amefanya kazialipokuwa chuoni, huenda asingepata kazi ya kitaaluma baada tu ya kuhitimu! Yote yalimsaidia, shukrani kwa bidii na azimio la Muji.
Huenda kukawa na mengi maishani mwako ambayo sasa hivi hayaendi jinsi ulivyokuwa umepanga, kama Kijana Muji, ni sawa kuhisi kuvunjika moyo, kukasirika, na kusikitika. Lakini, msichana, wewe ni wa nguvu na ndoto zako haziendi popote. Unaliweza hili, na tunakuamini!
Share your feedback