Rafiki yangu wa dhati alinisaidia kuamini talanta zangu
"Usaidizi Unahitajika Kwenye Tamasha za Kuigiza: Tunatafuta msanii wa vipodozi."
Tumbo langu liliruka niliposoma bango hilo. Nilihisi wasiwasi, lakini nilitaka kusaidia. Nilipenda darasa la sanaa na nilikuwa bora katika uchoraji wa picha, lakini ningeweza kuchora sura za watu? Kuwa msanii wa vipodozi wa tamasha ya shule ilikuwa jambo kubwa. Ilikuwa tamasha kubwa zaidi shuleni. Itakuwaje nikikosea? Kuchora picha katika darasa la sanaa lilikuwa jambo moja, lakini kuchora taswira ya kuonekana na kila mtu? Hili lilionekana la kuogofya.
Nilikuwa karibu kusahau wazo lile ambapo rafiki yangu wa dhati Lola - aliyekuwa muigizaji mkuu kwenye mchezo ule - alinikujia toka nyuma.
“Unawaza kuhusu nini Nadia?” aliniuliza kwa sauti yenye furaha.
“Ah hakuna” nilidanganya, lakini Lola alinijua vyema.
“Ninajua uso huo wako... Unawaza sana tena.”
“Basi...Sawa,” niligugumiza. “Nina wazo la kushangaza. Nilidhani nitasaidia na vipodozi vya mchezo ule.”
"Ah, Nadia. Safi kabisa!” Karibu Lola apige ukemi. Aliniambia kuwa nilikuwa msanii bora zaidi aliyejua na ingenibidi nifanye vile.
“Kuja nyumbani kwangu baada ya shule na nitakusanya baadhi ya waigizaji. Kuja na rangi zako na nitauliza mamangu kama tunaweza kutumia baadhi ya vipodozi vyake. Ninakuamini, Nadia. Unaweza!”
Nilipokuwa naenda nyumbani kwa Lola, nilihisi woga na nikatamani singekubaliana na mpango huu. Hata hivyo, nilipowasili waigizaji watatu walikuwa tayari wananingoja na walikuwa na tabasamu kubwa usoni mwao. Singeweza kujiondoa sasa! Rafiki yangu Edo aliashiria kimeza kidogo na juu yake kulikuwa na bango lililosema: "Studio ya ajabu ya Vipodozi ya Nadia. "
Mmoja baada ya mwingine, waigizaji wale walinionyesha picha ya muundo wa vipodozi walivyotaka na nikaanza kuwachora. Siku hiyo nilimgeuza mvulana mmoja kuwa simba, Lola akawa Malkia mrembo na nikafanya maajabu kubadilisha msichana mmoja mkubwa kuwa mchawi muovu aliye na uso wa kijani. Nilipata raha sana hadi nikasahau nilikuwa na woga!
Hii ndiyo siku marafiki zangu waliniamini sana hadi nikaanza kujiamini mwenyewe. Shukurani kwa marafiki zangu sasa ninafuata ndoto zangu.
Sasa ninajua mimi ni mtaalamu wa vipodozi!
Share your feedback