Wiki chache zilizopita, nilipata habari za kufurahisha kuwa nitakuwa kiranja. Nilikuwa nimesubiri wakati huu tangu nilipokuwa mtoto. Nilitaka kuwapa motisha wanafunzi wenzangu na kuwatia moyo ili wajiamini. Haikuwa rahisi kwangu wakati wote na nilitaka kushiriki hadithi yangu na wasichana katika mazingira yangu ili kuwaonyesha kuwa chochote kinawezekana. Sote tulikutanika katika uwanja wa shule mchana mmoja na niliwaelezea hadithi yangu.
Kama msichana mdogo, nilitatizwa na kusoma. Jambo hili lilinifanya kuwa mwenye huzuni na hata baadhi ya wanafunzi wenzangu darasani waliniita mjinga. Siku moja niliamua kuzunguza na mwalimu wangu kuhusu jinsi nilivyojisikia. Nilikua na ndoto za kuwa kiongozi katika jumuiya yangu, lakini jambo hili lilikuwa linanizuia. Jina lake lilikuwa Bi Dlamini na alikuwa mwanamke mkarimu zaidi niliyemfahamu. Nilimwambia kuwa nilijiona kuwa mjinga na kuwa nilitaka kusoma, lakini lilikuwa tatizo kwangu. Aliniambia kuwa hamna mtoto yeyote ambaye ni mjinga na kuwa sote hujifunza kwa njia tofauti. Aliamua kuanzisha darasa la kusoma la baada ya vipindi vya shule kwa watoto waliokuwa na matatizo ya kuelewa na akafanya masomo kuwa kitu cha kufurahia kwetu.
Alinifanya nijihisi mwenye ujasiri na kunionyesha kuwa ni muhimu kuzungumza kuhusu malengo na ndoto zako na mtu unayemwamini.Sisi sote tuna safari ya maisha na Bi Dlamini alinipa ujasiri wa kufuata safari yangu.
Iwapo unajiamini na kufanya kazi kwa bidii unaweza kufanikiwa katika kitu chochote. Kuzungumza na Bi Dlamini kuhusu uoga wangu ni chaguo bora zaidi nililofanya. Ni kiongozi wa ajabu na nina matumaini ya kuwa mkarimu na mwenye msaada kama jinsi alivyokuwa nitakapokuwa mwalimu siku moja. Zungumzia uoga na ndoto zako kila wakati kwa sababu itakufanya ujihisi vizuri! Kuna msaada mwingi zaidi ulimwenguni na kuna watu wengi zaidi wakarimu ambao wanataka kukusaidia.
Share your feedback