LAKINI, nina jambo jingine la kusema
Jina langu ni Janet na nilihamia mji mwingine hivi majuzi. Wazazi wangu walihamia huku kwa sababu ya kazi, kwa hivyo ilinibidi kuwacha marafiki zangu na nianze upya katika shule nyingine.
Siku yangu ya kwanza shuleni, nilikuwa na wasiwasi sana kupata marafiki wapya, lakini nilipatana na kijana huyu aitwaye Fred. Alinijia wakati wa chakula cha mchana na akanialika nijiunge na marafiki zake kwenye benchi. Aliniambia kila kitu nilichohitaji kujua kuhusu shule ile : walimu wazuri, wale wakali, jinsi ya kuzungumza vyema na mwanamke anayegawa chakula cha mchana ili aniwekee chakula kingi na wanapokaa wenye fitina. Nilianza kula chakula cha mchana naye na marafiki zake kila siku na wakati mwingine tungeenda nyumbani pamoja.
Siku moja, nilipokuwa nikienda shule na kundi la marafiki wa darasa langu, msichana aitwaye Eneka aliniuliza, “Ulikuwa utuambie lini kwamba wewe ni mpenzi wa Fred?” Nilishtuka sana! Nilikuwa namtamani Fred kiasi. Hata hivyo, hakuwa mpenzi wangu. Nilimuuliza alikopata habari zile na akaniambia kwamba alimsikia Fred akizungumza na wavulana wengine katika somo la Hesabu.
Nilikasirika sana hadi sikuweza kuzungumza tena safari yote iliyobaki. Awali, sikutaka kuzungumza na Fred tena, lakini nilipomuona wakati wa chakula cha mchana, niligundua kwamba ni muhimu nieleze maoni yangu. Kwa hivyo nilienda kwake na mbele ya marafiki zake wote, nikamwambia nilichokisikia na nikamhakikishia kwamba mimi sio mpenzi wake. Niliendelea kwa kumwambia kwamba asipowaambia watu ukweli, tutawacha kuwa marafiki.
Alikubali ukweli kwa marafiki zake na wakamkejeli kwa wiki kadhaa. Hata baada ya hili, bado nilikuwa nimekasirika naye. Sipendi watu wakinikatia kauli, nina akili zangu mwenyewe. Na kama angengoja, hakuna anayejua, labda tungekuwa wapenzi sasa. Lakini hakungoja, na hiyo ni hasara kwake.
Share your feedback