Usifanye mambo haya 3 wakati wa hedhi yako...

Ni wakati ule wa mwezi tena

Ndiyo, ni wakati ule wa mwezi tena lakini hedhi zote hazifanani. Pia hutapata hisia sawa katika hedhi zako. Miezi mingine itakuwa shwari. Miezi mingine itakuwa na uchungu.

Lakini usitie shaka; hivi hapa ni vidokezo 3 vya kukuongoza unapopata hedhi yako ili iwe shwari iwezekanavyo.

Usile chakula kilicho na mafuta mengi, chumvi nyingi na kilicho na sukari nyingi

Vyakula hivi vinajulikana kwa kuongeza uchovu, kufura tumbo, wasiwasi na mihemko ya hisia. Vinaweza kufanya matiti yako yawe mororo sana. Kitu kingine cha kuepuka? Bidhaa zinazotokana na maziwa. Maziwa yana calcium nyingi na virutubishi. Lakini sio mazuri kwako wakati wa hedhi kwa sababu yanaongeza gesi na maumivu ya tumbo. Kwa hivyo, ni vyema kuepuka maziwa hadi hedhi yako iishe. Ndiyo, kuepuka baadhi ya vyakula hivi si rahisi – hasa kama unavipenda. Lakini unaweza.

Kula samaki, mboga na matunda

Zitainua hisia zako na ziboreshe afya yako. Kunywa kikombe cha chai moto iliyo na tangawizi na/au asali pia. Itasaidia kupunguza uchungu wa hedhi. Kama unatoka damu nyingi, kula vyakula vilivyo na iron kama maharagwe na mboga ili kukupa nguvu. Pia, kunywa maji mengi ili uwe na kiwango kizuri cha maji mwilini.

Usiepuke kuoga na kujisafisha

Katika baadhi ya maeneo wasichana huambiwa wasioge wakati wa hedhi kwa sababu hii inaweza sababisha uchafuzi wa mazingira au utasa, lakini hili si kweli. Ni moja ya hadithi za uongo kuhusu hedhi.

Oga mara kwa mara na uwe safi Unapokuwa katika hedhi zako ni muhimu zaidi kuhakikisha uko safi na uoshe uke wako na maji. Hii itahakikisha hupati harufu yoyote mbaya au bakteria mbaya. Pia unafaa kubadilisha kisodo chako kila masaa 2-4 na uvitupe kama unaweza. Kama sio vya kutupa, jaribu kuviosha na kuvikausha mara kwa mara.

Usivae nguo nyeupe

Kama umezoea kupata madoa wakati wa hedhi yako, epuka nguo nyeupe au zilizo na rangi angavu. Hivi, hutahitajika kujiangalia nyuma kila wakati. Unastahili amani ya akili wakati wa hedhi.

Vaa nguo zisizo angavu

Zitatuliza nafsi yako na ziongeze imani yako. Na ukipata doa, hakuna atakayejua. Halafu unaweza kuondoka kisiri na ubadilishe nguo zako ikihitajika.

Kumbuka, haujakingwa kutokana na mimba na magonjwa ya zinaa (STIs) ukifanya ngono wakati wa hedhi yako.

Una maswali yoyote? Zungumza na mtu mzima anayeaminika kama vile dada mkubwa, shangazi au mtaalamu wa afya aliye na ujuzi.

Share your feedback